Muungano wa Kipekee Zaidi Duniani!

Published: April 28, 2020, 8 a.m.

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Muungano wa Nchi huru mbili zilizojulikana kama Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya watu wa Zanzibar. Nchi hizi mbili ziliingia kwenye Mkataba wa Muungano mnamo tarehe 22 Aprili, 1964 na kuwa Dola ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuanzia tarehe 26 Aprili, 1964. Muungano huu ni wa serikali mbili, yaani Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (SMT) inayoshughulikia mambo yote ya Muungano kama yalivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 na yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Bara na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) inayoshughulikia mambo yasiyo ya Muungano kwa upande wa Tanzania Zanzibar.

Mkataba wa Muungano ulitiwa sahihi na aliyekuwa Rais wa Tanganyika, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na aliyekuwa Rais wa Zanzibar, Hayati Sheikh Abeid Amani Karume tarehe 22 Aprili, 1964 huko Zanzibar.  Mkataba huo ulithibitishwa tarehe 26 Aprili, 1964 na mnamo tarehe 27 Aprili, 1964, viongozi wa nchi zote mbili walikutana katika ukumbi wa Karimjee, Dar es Salaam na kubadilishana hati za Muungano. Sheria za Muungano zilitoa tamko la Jamhuri ya Muungano kwamba:

“Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar zitalazimika, baada ya kuungana na siku zote baada ya kuungana, kuunganishwa kuwa Dola ya Jamhuri kwa jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar’ (Ibara ya 4 Sheria za Muungano)

Jina hili la “Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar” lilibadilishwa baadae na kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitia sheria ya Jamhuri ya Muungano, Sheria namba 61 ya mwaka 1964.